WALIMU WA AWALI NA MSINGI WATAKIWA KUWA CHACHU YA MABADILIKO MATUMIZI YA TEHAMA SHULENI
Angela Msimbira, TABORA
Serikali imeeleza kuwa katika zama za Maendeleo ya Sayansi na Teknolojia matumizi ya TEHAMA katika ufundishaji na ujifunzaji ni nyenzo muhimu itakayorahisisha utoaji wa elimu bora kwa ufanisi nchini.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uthibiti ubora wa shule kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Eprahim Simbeye kwenye Mafunzo ya TEHAMA kwa Walimu wa Shule ya awali na Msingi Tanzania Bara yanayofanyika katika Chuo cha Ualimu Tabora, mkoani Tabora.
Simbeye anaeleza kuwa kumekuwa na matumizi makubwa ya TEHAMA katika ujifunzaji na ufundishaji hivyo ni muhimu kwa walimu kuendana na mabadiliko hayo ili kuendana na malengo ya Serikali ya kutoka elimu bora na kwenda na mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia zinazoendele duniani
“ Matumizi yaTEHAMA ni muhimu kwa sasa, matumizi ya karatasi na kuandika vinapotea, hivyo ni muhimu kupata ujuzi na maarifa kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA katika ujifunzaji na ufundishaji nchini,” amesema Simbeye.
Amesema kuwa ni wajibu wa kila mwalimu kutumia vifaa walivyonavyo katika ufundishaji na ujifunzaji hasa matumizi sahihi ya vishikwambi pamoja na kompyuta kwa ajili ya kufundishaili kuendana na mabadiliko ya teknolijia.
“Tumieni vishikwambi mlivyopatiwa na Serikali kwa ajili ya kufundisha na kupata maarifa badala ya kuvitumia kinyume na utaratibu,” amesisitiza Simbeye.
Amewataka walimu hao kuhakikisha wanaitendea haki katika kuhakikisha wanatumia ujuzi walioupata katika kuwafundisha wengine juu ya matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA shuleni.
Simbeye amewataka walimu hao kuhakikisha wanakuwa chachu ya mabadiliko kwenye vituo vyao vya kazi kwa kuhakikisha wanafundisha na kusimamia maadili bora kwa wanafunzi ili kujenga taifa lenye maadili.
Mafunzo kuhusu matumizi sahihi ya vifaa vya TEHAMA na vishikwambi katika kufundisha na kujifunza kwa walimu wa shule za awali yanasimamiwa na Wizara.