Habari

Mawaziri wa Kundi la Nchi zilizoendelea kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi wameazimia kuwa na Msimamo wa Pamoja katika Masuala Muhimu

0:00

Mawaziri wa Kundi la Nchi zilizoendelea kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi wameazimia kuwa na Msimamo wa Pamoja katika Masuala Muhimu yatakayojadiliwa katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.

Mkutano huo ulioanza Septemba 28 hadi 29, 2023 jijini Dakar, Senegal umehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira). Mhe. Dkt. Selemani Jafo.

Akizungumzia mkutano huo, Waziri Jafo amesema yaliyojadiliwa ni tathmini ya kidunia kuhusu utekelezaji wa Makubaliano ya Paris unaosisitiza haja ya kuchukua hatua za haraka na madhubuti kuepuka kuongezeka kwa athari na kiwango cha ongezeko la wastani la joto duniani kuvuka nyuzijoto 1.5.

Pamoja na kiwango cha fedha za mabadiliko ya tabianchi kuongezeka imebainishwa bado ni kidogo na hakikidhi mahitaji hivyo, iliazimiwa kuwa matokeo ya tathmini hiyo yawe chachu ya upatikanaji wa fedha hizo.

Aidha, Dkt. Jafo amesema kuwa mkutano ulibainisha kuwa ahadi ya nchi zilizoendelea ya ukusanyanyaji wa Dola za Marekani Bilioni 100 ifikapo mwaka 2025 haijatimizwa, hivyo uhaba wa fedha ni changamoto kwa nchi zinazoendelea na hazikidhi mahitaji ya kukabiliana na changamoto zilizopo.

Kutokana na hali hiyo iliazimiwa kuwa taratibu za upatakanaji wa fedha kutoka katika Mifuko ya Mabadiliko ya Tabianchi zirahisishwe, kutimizwa kwa ahadi ya nchi zilizoendelea ya ukusanyaji wa fedha za mabadiliko ya tabianchi na umuhimu wa kuongeza kiwango cha fedha kukidhi mahitaji.

Dkt. Jafo amesema kuwa majadiliano hayo pia yalijikita kuhusu muundo wa Mfuko wa Kushughulikia Hasara na Uharibifu Utokanao na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, taasisi itakayosimamia Mfuko, vyanzo vya fedha na utaratibu wa upatikanaji wa fedha kwa nchi zitakazokidhi vigezo.

Back to top button