MAMA MARIAM MWINYI AMETOA WITO KWA JAMII KUTUMIA MBINU ZA KUIMARISHA LISHE
Mke wa Rais wa Zanzibar, Msarifu na Mwenyekiti wa bodi ya wadhamini Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation (ZMBF) Mhe.Mama Mariam Mwinyi ametoa wito kwa jamii kutumia mbinu mbalimbali za kuimarisha lishe kwa watoto na mama wajawazito ambazo zitachangia hatua za awali za ukuaji wa mtoto tangu mimba inapotunga, wakati wa ujauzito na baada ya kuzaliwa hadi kufikia umri wa miaka miwili.
Mama Mariam Mwinyi amesema hayo katika mkutano wa wadau wa masuala ya afya na lishe kupitia mradi wa lishe unaotekelezwa kwa mashirikiano kati ya Wizara ya Afya Zanzibar, Taasisi ya Benjamin Mkapa na Taasisi ya Zanzibar Maisha Bora Foundation kwa udhamini wa Shirika la Chakula Duniani (WFP) ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Airport tarehe: 02 Februari 2024.
Aidha Mama Mariam Mwinyi amesema ZMBF imekuwa ikitekeleza shughuli mbalimbali zinazohusiana na afya nchini hususani afya ya uzazi kwa vijana balehe na kuzuia maradhi yasiyo ambukiza.
Vilevile Mama Mariam Mwinyi ameeleza kuwa kuanzia tarehe 4 hadi 8 mwezi Machi mwaka huu , Taasisi ya ZMBF ikishirikiana na Wizara ya Afya Zanzibar itaendesha kambi ya matibabu ya afya bure na kuwafikia wananchi wengi zaidi kupitia kampeni ya Afya Bora, Maisha Bora.
Mama Mariam Mwinyi ametoa wito kwa Wizara ya Afya kuhakikisha elimu ya afya ya lishe inatolewa katika ngazi ya jamii kupitia wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao kwa Zanzibar wanapatikana kila kaya.