Habari Tofauti

MAAFISA USTAWI WAPATA ELIMU JUU YA UWIANO WA  KIJINSIA.

Serikali imesema ili kuhakikisha kuna uwiano wa kijinsia katika upatikanaji wa huduma imeandaa mwongozo wa uwiano wa kijinsia ili makundi  yote yashiriki katika maendeleo ya jamii lakini pia kuondoa ukatili.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju wakati akizungumza na Maafisa Ustawi wa Jamii wa Wizara za Kisekta, Taasisi za Umma na wadau kwenye mafunzo ya utoaji wa huduma kwa kuzingatia uwiano wa kijinsia ili kufikia kizazi cha usawa, yaliyofanyika jijini Dodoma Agosti 31,2023.

“Mwongozo huu umelenga kutekeleza makubaliano ambayo Tanzania imeridhia katika mikataba yake ya kimataifa lakini pia katiba yetu ya Tanzania inaelekeza kutoa huduma kwa watu wote bila ubaguzi wowote“ amesema Mpanju.

Wakili Mpanju amewasisitiza Maafisa Ustawi hao kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili maarifa yote yanayopatikana yatumike nchi nzima ili lengo la  Serikali kuwa na jamii yenye usawa litimie.

Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando amesema mwongozo huo umeandaliwa kupitia hatua kadhaa ikiwemo vikao kadhaa na kufanyiwa majaribio kadhaa  na wadau na kupitia mafunzo mbalimbali hadi kufikia hatua ya ukamilishaji.

“Malengo ya Semina hii ni kutoa uenezi  wa mwongozo huu kwa maafisa ustawi  ili utumike nchi nzima  na ukazibe mapengo yote yaliyokuwepo kwenye uwiano wa kijinsia nchi nzima” amesema Dkt. Nandera.

Naye Mkurugenzi Msaidizi kutoka Ofisi ya Rais  TAMISEMI Subisya Kabuje amesema mwongozo huo utafanikiwa zaidi endapo utasambazwa kwa Maafisa Ustawi wote kutoka mikoa yote na Halmashauri zote na kusaidia kutatua changaoto zilizokuwepo.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Shirika la PACT Tanzania Flora Nyagawa amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana  kikamilifu na Wizara kuhakikisha afua zote zinatekelezwa ili kuwa na Taifa lenye uwiano wa jinsia.

زر الذهاب إلى الأعلى