Habari Tofauti

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa amewahimiza Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 Bw. Abdalla Shaibu Kaim amewahimiza Watanzania kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhifadhi mazingira.

Bw. Kaim ametoa kauli hiyo za wakati akiongoza zoezi la upandaji wa miti katika Shule ya Sekondari Kifaru wakati Mwenge wa Uhuru ulipowasili wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya kukagua miradi ya maendeleo.

Ametoa wito kwa wananchi kupanda miti hatua itakayosaidia kuhifadhi mazingira na hivyo kusaidia katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinazokabili maeneo mbalimbali nchini.

“Ndugu zangu wana Mwanga nichukue fursa hii kuwapongeza kwa zoezi hili la upandaji ikiwa ni hatua za kuunga mkono jitihada za Serikali na ujumbe wa Mbio za Mwenge mwaka huu, niwaambie kazi mnayofanya ina tija na afya kwa taifa letu,” amesema Kaim.

Katika mbio hizo, kiongozi huyo pia amekagua na kuzindua maeneo ya utunzaji wa mazingira na uokoaji wa vyanzo vya maji ambapo ameupongeza uongozi wa Bonde la Pangani kwa kuutendea haki ujumbe wa Mwenge.

Mwenge wa Uhuru unaendelea kukimbizwa katika mikoa mbalimbali nchini ambapo ujumbe wa mwaka 2023 ni “Tunza Mazingira, Okoa vyanzo vya Maji kwa Ustawi wa Viumbe hai na Uchumi wa Taifa”.

Kutokana na umuhimu wake zoezi la utoaji wa elimu ya uhifadhi wa mazingira inaendelea kutolewa kwa wananchi wanaojitokeza katika maeneo mbalimbali Mwenge wa Uhuru unakopita

زر الذهاب إلى الأعلى