Habari

Dkt. Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Standard Chartered

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amekutana na kufanya mazungumzo na Afisa Mtendaji Mkuu wa benki ya Standard Chartered, Bw. Herman Kasekende na kujadili fursa za uwekezaji na uwezeshaji wa miradi ya mazingira na uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi hapa nchini.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Ofisi ndogo za Ofisi ya Makamu wa Rais Jijini Dar es Salaam, leo Oktoba 10, 2023, Waziri Jafo ametoa wito kwa benki hiyo kuweka mpango na mikakati madhubuti ya uwekezaji katika nishati safi ya kupikia ili kuepusha uharibifu wa mazingira.

Amesema kuwa nishati ya kupikia isiyo salama kwa matumizi ikiwemo kuni na mkaa imekuwa na madhara kwa afya kwa watumiaji sanjari na kuharibu mazingira.

“Serikali imendaa rasimu ya Dira ya Taifa ya Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia 2033…Tunaendelea kuwahimiza wadau ikiwemo taasisi za kifedha kujitokeza na kuwekeza katika miradi ya uzalishaji wa bidhaa na nishati safi ya kupikia na hivyo kurahisisha upatikanaji wake kwa Watanzania,” amesema Dkt Jafo.

Aidha, Waziri Jafo ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa benki hiyo kwa juhudi zake katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi hapa nchini.

Katika hatua nyingine Dkt. Jafo amesema mapambano ya uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi yanahitaji juhudi za pamoja baina ya serikali na wadau na kutokana na umuhimu huo, Serikali imeendelea ushirikiano na wadau wa maendeleo ikiwemo taasisi za kifedha ili kuibua fursa za uwezeshaji na uwekezaji wa miradi ya mazingira nchini.

Amesema Serikali imeandaa kanuni na mwongozo kuhusu biashara ya kaboni ikiwa ni mkakati wa kuboresha usimamizi mzuri wa miradi ya biashara ya kaboni inayotekelezwa nchini, na kuzitaka taasisi za kifedha kujitokeza katika kuziwezesha mitaji kwa kampuni mbalimbali za Watanzania.

“Utekelezaji wa biashara ya kaboni utachangia kupunguza gesijoto na hatimaye kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na pia kuchangia katika utunzaji endelevu ya mazingira na kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi kwa wananchi wetu..Jukumu hili linahitaji mshikamano wa wadau wote,” amesema Dkt. Jafo.

زر الذهاب إلى الأعلى