Habari Tofauti

DKT. BITEKO AKUTANA NA WAZEE NA VIONGOZI WA DINI WILAYANI BUKOMBE

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa dini kutoka madhehebu mbalimbali wilayani Bukombe pamoja na Wazee wa wilaya hiyo, katika mkutano uliolenga kubadilishana mawazo na kumshukuru Mungu kwa mwaka 2023.

Mkutano huo umefanyika tarehe 31 Desemba 2023, Ushirombo wilayani Bukombe mkoani Geita na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama cha Mapinduzi na Serikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed ambaye kwa sasa anakaimu nafasi ya Ukuu wa Wilaya ya Bukombe.

“Mimi pamoja na wenzangu serikalini tunawashukuru sana wazee na viongozi wa dini wa Bukombe kwa ushirikiano mkubwa mnaotoa kwetu, leo nimeona tupate nafasi ya kumshukuru Mungu pamoja na ninyi  na kubadilisha mawazo kwani hakuna kiongozi anayeweza kufanya jambo  lolote bila kushirikishana na wenzake, ninyi mmeona mengi kuliko mimi, mnafahamu mengi, mnajua mengi, uelewa wenu ni mkubwa na pia mnakaa na jamii muda wote hivyo mnafahamu wapi turekebishe ili tutengeneze Bukombe bora zaidi.” Amesema Dkt. Biteko

Ili kuwa na jamii iliyo bora, Dkt. Biteko amewaasa viongozi hao wa dini na wazee kuendelea kukemea matendo mabaya pale wanapoyaona, tena bila kuyaonea aibu  kwani ni watu wanaoheshimika katika jamii na ujumbe kutoka kwao unawafikia watu wengi.

Pamoja na kueleza  utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Bukombe ikiwemo Shule, Vituo vya Afya, Hospitali, usambazaji umeme na barabara, Dkt. Biteko  amesema kuwa, changamoto zozote ambazo bado zipo wilayani humo zitatatuliwa ili Bukombe iweze kuwa bora zaidi.

Katika mwaka 2024, Dkt. Biteko ametoa ujumbe wa watu  wa makundi yote kupendana na kusameheana na kwamba Serikali itaendelea kuhakikisha inatoa huduma bora kwa wananchi ili watoto wasome kwenye shule nzuri, wananchi watumie barabara nzuri, wahudumiwe katika zahanati, kituo cha afya na  hospitali nzuri, wapatiwe huduma ya umeme na maji hali itakayofanya pia watu kupenda maeneo walikotoka.

زر الذهاب إلى الأعلى