Habari

Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akutana na Watanzania wanaoishi Cairo

0:00

Tarehe 21 Machi, 2024 Mhe. Mej. Jen. Richard Mutayoba Makanzo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri alikutana na Watanzania wanaoishi Cairo nchini Misri kwa lengo la kufahamiana na kupeana nasaha.

 Hafla hiyo iliyowahusisha Maafisa wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Jeshi la Polisi, Mapadre na Vijana wanaosoma vyuo na kozi mbali mbali.

Pia, walihudhuria Watanzania mbali mbali wanaoishi Cairo, wanaofanyakazi katika Vyuo Vikuu na Taasisi mbali mbali.

 Mhe. Balozi aliwanasihi Watanzania hao kufuata sheria za nchi kwa kuwa na Vibali halali vya kuishi ili kuepuka operesheni kamatakamata inayoendelea dhidi ya wageni wanaoishi kinyume na sheria kwa kutokuwa na visa na hati za kusafiria.

Aidha, aliwataka kuwa na umoja imara, katiba inayofuatwa kikamilifu na kufanya mikutano kila baada ya muda kujadili mambo mbali mbali yenye maslahi kwao na nchi kwa ujumla.

Aliwasisitiza kufika ubalozini na ubalozi upo kwa ajili yao, kwa shida na raha. Naye Mwenyekiti wa Diaspora waliopo Misri Bw. Fadhili Mansour aliupongeza ubalozi kwa kuwa nao karibu katika shida na raha na kuwakutanisha Watanzania katika hafla hiyo muhimu na kupata chakuka cha pamoja mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Alieleza kuwa Hadi sasa Watanzania wawili walikamatwa na Polisi, mmoja amesharejeshwa Tanzania na mwengine yuko kituo cha Polisi akisubiri maamuzi ya vyombo vya usalama, kwa kuendelea kubakia nchini Misri au kurejeshwa Tanzania.

 Nae Bw. Haroun Rashid, mlezi wa Diaspora aliwanasihi Watanzania kuhalalisha ukaazi wao na kuacha kujificha, kwani hakutawasaidia.

Hivyo, aliwataka wjitahidi kupata vibali halali vya kuishi na ikishindikana kabisa, ni vyema kufanya uamuzi wa kurejea Tanzania kuepuka msako unaoendelea kwa wageni wanaoishi kinyume na sheria na taratibu za Nchi ya Misri.

Back to top button