Habari

WAZIRI MKUU AKUTANA NA WAWEKEZAJI WA URUSI

Awahakikishia mazingira rafiki kwa mitaji yao

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na wawekezaji kutoka kampuni nne za Urusi zenye nia ya kuwekeza nchini katika nyanja ya usindikaji mazao, nishati jadidifu na utengenezaji wa vifungashio vya glasi.

Kampuni hizo ni SEIES (usindikaji mazao na mitambo yake), Agrovent (kusindika mazao yanayoharibika haraka), Unigreen Energy (Nishati Jadidifu) na TD Glass NN Expo LLC (utengenezaji wa chupa za vioo vya kutumia mchanga na magadi).

Amekutana nao leo (Jumamosi, Julai 29, 2023) kwa nyakati tofauti wakati akizungumza nao jijini St. Petersburg, Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.

Akielezea kuhusu kampuni yao, Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni ya SEIES, Bw. Yuri Korobov amesema wanasindika vyakula kwa kukausha mazao bila kuharibu viinilishe (nutrients) na vyakula hivyo vinaweza kuhifadhiwa kwa mwaka mmoja.

“Tukianzisha mradi huu tunaweza kuhifadhi matunda na vyakula vingi vilivyoko Tanzania. Tunatumia teknolojia ya kugandisha na kukausha maji yote bila kuharibu viinilishe. Mradi huu unaweza kupanuliwa katika wilaya na mikoa mingine nchini Tanzania kwani tumelenga wakulima walioungana kwenye vyama vya ushirika,” amesema.

Bw. Korobov ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Kuratibu Biashara za Taasisi za Umma nchini Urusi (Delovaya Rossiya) alisema wamepanga kuwafundisha wafanyakazi ili wawe na elimu ya uhandisi wa kusindika mazao hayo.

Delovaya Rossiya ambayo pia ni maarufu kama “Business Russia” ilianzishwa mwaka 2001, inaunganisha wafanyabiashara zaidi ya 7,000 na ina uwakilishi kwenye majimbo yote 85 ya Shirikisho la Urusi.

Kwa upande wake, Mmiliki wa Kampuni ya SEIES, Bw. Mikhail Mikhailov alisema kampuni hiyo pia inabuni ufundi na kutengeneza vifaa vinavyotumika kwenye teknolojia ya kukausha mazao. “Nchi zinazoongoza kwa teknolojia hii ni China na Uturuki, tunaamini Tanzania inaweza kushindana nao na kuwa mbele zaidi kwenye teknolojia hii.”

Back to top button