Habari

SERIKALI KUTENGA FEDHA KULINDA HADHI YA URITHI WA MJI MKONGWE ZANZIBAR

Ahmed Hassan

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi amewataka Wananchi waelewe dhamira ya Serikali ni  kuhakikisha Mji Mkongwe unabaki kama ulivyokuwa miaka mia mbili iliyopita na si kuubadilisha  .Aliyasema hayo katika hafla fupi ya ufunguzi wa Jengo jipya la Hoteli ya Tembo, iliyofanyika Ukumbi  wa Tembo House Hoteli ,Shangani leo tarehe 22 Machi 2023 Mkoa wa Mjini Magharibi.

Rais Dk.Mwinyi amesema wapo wanaojaribu  kupotosha kuwa Serikali ina lengo la kuubadilisha Mji  Mkongwe kwa kuugawa na  kubinafsisha  na akaeleza lengo ni kuwapa watu wenye uwezo kuyajenga majengo hayo , kuyatunza ili yaweze kudumu miaka  mia mbili ijayo akitolea mfano Jengo la sasa la Tembo Hoteli lilikuwa Ubalozi wa Marekani mwaka 1831 na Jengo lililozinduliwa leo kwa marekebisho ilikuwa ni Skuli mwaka 1944.

Aidha, Rais Dk.Mwinyi amewakaribisha  wawekezaji  waje kushirikiana na Serikali  kurudisha hadhi ya Mji Mkongwe na kuujenga huku akitoa miezi mitatu kwa waliopewa Majengo mbalimbali kwa ajili ya kuyarekebisha na kuyaendeleza wakishindwa Serikali itayachukua  .Pia ameeleza  Serikali imeamua kutenga fedha kuhakikisha inaleta mfumo bora wa maji,  mfumo wa kisasa wa umeme , huduma ya Internet,  ujenzi wa barabara katika Mji Mkongwe ili kuwa kivutio kwa utalii .

Vilevile, Rais Dk.Mwinyi  amemshukuru Mfalme wa Oman Sultan Haitham Bin Tariq M Said na Serikali yake kwa msaada wa Dola za Kimarekani Milioni 21 kwa ajili ya ujenzi wa Jengo la Beit-al-Ajaib na kulirudisha katika hadhi yake na mkandarasi ameshapatikana  na ujenzi utaanza hivi karibuni.

Back to top button