Takriban vijana 80,000 wanatarajiwa kukutana na Papa, ambaye analenga kuendelea kusambaza ujumbe wa amani na maridhiano baada ya jana Jumatano kukutana na wahanga wa madhila ya machafuko ya nchini humo.
Maelfu ya vijana walianza kuingia katika Uwanja wa Mashahidi ulioko mjini Kinshasa mapema hii leo tayari kabisa kwa mkutano wa hadhara utakaoongozwa na kiongozi huyo wa kiimani.
Uwanja huo unatarajiwa kufurika vijana kama 80,000 hivi ili kusikia ujumbe utakaotolewa na Papa, aliyeko ziarani barani Afrika.
Karibu asilimia 60 ya watu nchini humo ni vijana wa chini ya miaka 20, hii ikiwa ni kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa. Pamoja na mzozo unaoendelea kuwaathiri vijana, wengi pia hawana ajira. Sheila Magumbu, mmoja ya vijana waliojitokeza uwanjani hapo amesema anatumaini kusikia ujumbe wa amani kutoka kwa Papa Francis, na hasa kwa ajili ya wakazi wa mji wa Goma ulioko mashariki mwa Kongo.
Na kama ilivyo kwa Sheila, wengi wanaamini kwamba huo ndio utakuwa ujumbe mkuu ikiwa ni pamoja na maridhiano miongoni mwa watu wa taifa hilo ambalo mizozo imesababisha mamilioni ya watu kuuawa katika miongo kadhaa iliyopita, huku watu milioni 5.7 wakiwa hawana mahala pa kuishi baada ya kuyakimbia makazi yao.
Hapo jana, Papa Francis alikutana na wahanga wa madhila ya machafuko nchini humo na kusikiliza visa vya kutisha na kusikitisha. Kulingana na vyombo vya habari, Papa alisikiliza kwa umakini mkubwa shuhuda zilizotolewa kuanzia za kijana aliyelazimika kutizama wakati baba yake akikatwakatwa viungo, kisa cha msichana mdogo kubakwa kama mnyama kwa miezi kadhaa na mtumwa wa zamani wa ngono aliyelazimishwa kula nyama za watu.