NDEJEMBI AELEKEZA KUREKEBISHWA MADIRISHA YA SHULE MPYA YA MSINGI KONA NNE
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Deogratius Ndejembi amemtaka fundi aliyepewa kandarasi ya kujenga shule mpya ya msingi ya Kona Nne iliyopo Halmashauri ya Wilaya Ushetu kurekebisha kwa gharama zake mwenyewe madirisha yote aliyoyaweka bila kuzingatia maelekezo ya Serikali.
Mhe. Ndejembi amemtaka fundi huyo kufanya marekebisho hayo haraka, wakati akikagua ujenzi wa miundombinu ya elimu katika shule ya mpya ya msingi ya Kona Nne inayojengwa kupitia mradi wa BOOST katika Kijiji cha Bugomba ‘A’ Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu ambapo alibaini dosari kwenye madirisha ya aluminium yaliyowekwa katika shule hiyo.
“Naelekeza ndani ya siku 14 madirisha yote yaondolewe ili marekebisho yafanyike kwa ufanisi tena kwa gharama za fundi na wasimamizi na si za Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu,” Mhe. Ndejembi amesisitiza.
Mhe. Ndejembi amesema amebaini madirisha hayo hayana wavu na hayajawekwa kwa viwango stahiki, hivyo marekebisho yafanyike na taarifa ya kukamilika kwa marekebisho hayo iwasilishwe kwa maandishi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu, Mkuu wa Wilaya ya Kahama na kwake ili kujiridhisha na utekelezaji wa maelekezo yake.
Aidha, amemtaka kamanda wa TAKUKURU wilaya ya Kahama kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha katika ujenzi wa shule hiyo ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa watakaobanika kukwamisha jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuboresha miundombinu ya elimu nchini.
Sanjari na hilo, amemtaka Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu Bi. Hadija Kabojela kuchukua hatua za kinidhamu Mwalimu Jonas Mabusi ambaye ni msimamizi wa ujenzi na aliyekuwa mkuu wa shule hiyo Bi. Stella Solezi kwa kushindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo.