Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais ameitaka jamii kupanda miti kuzunguka maeneo yenye miradi
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Switbert Mkama ameitaka jamii kupanda miti kuzunguka maeneo yenye miradi ili kuhifadhi mazingira na kuifanya kuwa endelevu.
Amesema hayo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Mradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Wilaya ya Kaskazini ‘A‘ Mkoa wa Kaskazini, Unguja – Zanzibar tarehe 19 Agosti, 2023.
Akikagua visima, ujenzi wa majengo ya vituo vya wajasiriamali wa ufugaji, ushonaji, utengenezaji wa sabuni pamoja na vitalu nyumba katika Shehia za Jugakuu, Mbuyutende na Kijini, Dkt. Mkama amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa.
Aidha, aliwahimiza viongozi wakiwemo masheha wa shehia hizo ambazo zimefaidika na miradi ya visima kuwasimamia wananchi kupanda miti na kuimwagilia.
“Binafsi nimeridhishwa na namna mnavyosimamia miradi hii na nawapongeza masheha kwa kuisimamia na wananchi kwa kuipokea na kushiriki kikamilifu katika kuitekeleza, niwaombe mhakikishe inaendelea kuwa na ubora ule ule,“ amesisitiza.
Kwa vile ujenzi wa majengo ya wajasiriamali wa ushonaji na uzalishaji wa sabuni utahusisha mashine na vifaa, Dkt. Mkama amesema ni muhimu kuwepo na mpango mkakati ili mradi uwe endelevu hata pale utakapokwisha muda wake.
Amesema vyerehani vitakavyotolewa pamoja na vifaa vingine vikiwemo taa na mabomba ya maji vitahitaji matengenezo madogo madogo na kulipiwa umeme hivyo wanajamii waangalie namna ya kuuhudumia bila kusubiri serikali.