Habari Tofauti

MILIONI 500 ZANUFAISHA WANANCHI 42,000 LIGANGA – LUDEWA

Wananchi zaidi ya 42,000 katika tarafa ya Liganga,Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa, mkoani Njombe wameanza kunufaika na huduma za matibabu ya kawaida na upasuaji  baada ya kukamilika kwa ujenzi wa kituo cha Afya Liganga kuwekewa vifaa tiba vya kisasa.

Ujenzi huo ulioanzishwa kwa nguvu za wananchi mwaka 2018 na Serikali kuongeza shilingi milioni 500 una miundombinu yote inayotakiwa kwenye kituo cha Afya.

Mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt.Godfrey Mlelwa ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kukamilisha kituo hicho kwani wananchi walikuwa wanalazimika kutembea zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma hizo.

“ Kituo chetu cha afya kimekamilika mwezi April mwaka huu kikiwa na majengo ya maabara,jengo la wagonjwa wa nje, jengo la kufulia ,chumba cha upasuaji na wodi ya kuijifungulia na kulaza.

Pia tunaishukuru Serikali imetupa shilingi milioni 150 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba na vingine tumenunua kwa mapato ya ndani.” Amesema Dkt.Mlelwa.

Kituo hicho kimeanza kutoa huduma za upasuaji Septemba 21,2023 wakati huduma zote za msingi kama uzazi,chanjo,maabara,huduma za VVU na wagonjwa wa nje zikiwa zimeanza tangu mwezi wa 4 mwaka huu.

Upasuaji huo wa kwanza hospitalini hapo umefanikiwa huku mama na mtoto wakiendea vizuri na ulifanyika chini ya madaktari  Dr .Flavian mgaya, Dr.Victor lyimo ,nesi Revina lugome  huku George mwakalasya  akiwa ni Mtalam wa usingizi.

زر الذهاب إلى الأعلى