Habari

MAUZO YA NYAMA NJE YA NCHI YAONGEZEKA

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema kuwa mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 1,774 mwaka 2020/2021 hadi kufikia tani 14,701 mwaka 2022/2023.

Amesema hatua hiyo imechangiwa na ushirikiano wa kibiashara na mataifa mbalimbali duniani uliohamasishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema hayo leo Jumatatu (Mei 13, 2024) wakati wa hafla ya uzinduzi na makabidhiano ya Kituo Atamizi cha Ufugaji wa Kibiashara kwa Vijana kilichopo Kongwa mkoani Dodoma. Kituo hicho ambacho ni maalum kwa ajili ya unenepeshaji wa mbuzi kimegharimu sh. bilioni 1.6.

“Masoko ya nyama yameendelea kuongezeka na  kuzifikia nchi 12 ambazo ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, UAE na Vietnam.”

Ameongeza kuwa nyama ya mbuzi imeendelea kuongoza katika mauzo ya nyama nje ya nchi ambapo imechangia asilimia 70.1 ya mauzo yote. “Hali hii inathibitisha kwamba mradi huu ambao tunakabidhiana leo una manufaa makubwa ya kiuchumi katika nchi yetu kwa kuwa nyama ya mbuzi ina uhitaji mkubwa ndani na nje ya nchi.”

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa vijana kuitumia fursa ya uwepo wa kituo hicho kwa manufaa yao binafsi na manufaa ya taifa kwa ujumla.

“Lengo la mradi unaokabidhiwa leo ni kuwapatia vijana ujuzi kwa vitendo ikiwemo elimu ya ujenzi wa mabanda, ulishaji, matibabu na usimamizi wa mradi wa ufugaji mbuzi lakini pia kutoa mafunzo ya biashara ili  wawe wajasiriamali na waweze kuendeleza biashara ya unenepeshaji mbuzi.”

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa wafanyabiashara na wasindikaji wa nyama washirikiane na kituo hicho ili kupunguza changamoto ya upatikanaji ya mifugo bora kwa ajili ya uzalishaji wa nyama na mazao yake.

زر الذهاب إلى الأعلى