WAZIRI MKUU AZURU VIJIJI VINNE VYA JIMBO LAKE
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Ruangwa (Alhamisi, Desemba 21, 2023) alifanya ziara kwenye vijiji vinne vya kata ya Mbekenyera, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Vijiji alivyovitembelea na kuzungumza na wakazi wake ni Chingumbwa, Mkutingome, Naunambe na Mbekenyera.
Akizungumza na wakazi wa kijiji cha Chingumbwa katika kata ya Mbekenyera, Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili, kata hiyo imepatiwa sh. bilioni 2.5 za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwemo ya sekta za afya na elimu.
Pia amewataka wakazi hao waendelee kuwa na imani na Serikali ya awamu ya sita kwani imedhamiria kutatua kero zao. “Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kushirikiana na wana-Ruangwa na Watanzania wote katika kutatua changamoto zilizopo hivyo endeleeni kuwa na imani naye, na muwe na imani na Serikali yenu ya awamu ya sita,” amesema.
Amesema kuwa Serikali itaendelea kusimamia kikamilifu ujenzi na ubora kwenye sekta ya elimu kuanzia shule ya msingi ili watoto wasitembee umbali mrefu kufuata shule.
Akiwa kwenye kijiji cha Mkutingome, Waziri Mkuu ameagiza RUWASA wilaya ya Ruangwa ikamilishe kwa wakati mradi wa maji utakaohusisha vijiji vya Chingumbwa na Mkutingome ili wananchi hao waanze kupata huduma ya maji safi na salama.
Ili kuharakisha kukalimika kwa mradi huo, Waziri Mkuu amesema: “Natambua kuwa ujenzi huo utahusisha uwekaji wa vilula, kazi hii msiitoe kwa mkandarasi mmoja, gaweni kazi, mmoja apewe chanzo tu, mwingine njia za maji na mwingine ajenge vilula,” amesema.
Akitoa maelezo kuhusu mradi huo, Kaimu Meneja wa RUWASA, wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Rashid Shabani amesema kuwa wanaendelea na taratibu za ujenzi wa mradi huo ambao unategemea kuzalisha zaidi ya lita 5,000 kwa saa.
Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, aliwasisitiza vijana wa kata hiyo watumie fursa ya uwepo wa madini ili kukuza uchumi wao na waende Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) ili wapate ujuzi na kuboresha stadi kwenye uchimbaji wa madini.