Habari

Waziri Jafo ahamasisha vijana kupiga vita mabadiliko ya tabianchi

0:00

 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo amewataka vijana duniani kote kushiriki katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amewataka kupaza sauti kwa pamoja na kuelezea wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la hasara na uharibifu unaohusiana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ametoa kauli hiyo alipofungua Kongamano la Tatu la Kimataifa la Viongozi Vijana na Mabadiliko ya Tabianchi (Global Youth Climate Summit) lililofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Jafo amewataka vijana kuwa mabalozi wa Kampeni ya nishati safi ya kupikia na teknolojia, kuendeleza usawa wa kijinsia kwa wanawake wa vijijini na vijana katika nchi zinazoendelea na kuchukua jukumu la kuhamasisha mabadiliko.

Pamoja na hayo pia, ameonesha umuhimu wa Mfuko wa Hasara na Uharibifu unafanya kazi haraka iwezekanavyo na kupatikana kwa nchi zote zinazoendelea.

“Kongamano hili ni jukwaa la kipekee vijana wenye ujuzi tofauti mnakutana kwa lengo la kuongeza uelewa wenu wa sayansi ya mabadiliko ya tabianchi, kukuza uongozi, na kutengeneza suluhisho zitakalopeleka kuzuia na kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi”

Aidha, Dkt. Jafo amewataka washiriki wa kongamano hilo kubadili mtazamo wao kutoka kwenye utayarishaji wa nyaraka kuwa vitendo kwenye ngazi ya jamii.

Amekipongeza Kituo cha Uongozi wa Vijana wa Kimataifa  kwa ushirikiano na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa juhudi zao za kuwawezesha vijana na kuwaandaa kukabiliana na changamoto za uchumi wa kijani na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu wa Tanzania (TFS) Prof. Dos Santos Silayo amesema kongamano hilo linalenga kujenga uwezo wa vijana na kuwaandaa viongozi katika mapambano ya mabadiliko ya tabianchi duniani.

Back to top button