Sheria ya Mipango Miji huzingatiwa kuzipa hadhi Mamlaka za Miji
Serikali imesema hatua za upangaji wa miji nchini hufuata mpango wa mji husika kwa kina kabla ya hupandisha hadhi kuwa Mamlaka ya Mji kamili.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Mheshimiwa Deogratius Ndejembi Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI Bungeni Jijini Dodoma leo wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Vijijini Mheshimiwa Daniel Baran Sillo aliyetaka kujua ni lini Serikali itaupandisha hadhi Mji mdogo wa Magugu kuwa Mamlaka ya Mji.
“kusudio la kupandisha hadhi Mji wa Magugu lipo katika hatua za upangaji wa miji ikiwemo Uandaaji wa Mpango wa jumla na Mpango wa kina ambapo ikikamilika itatangazwa kupitia gazeti la Serikali”
Aidha, Mheshimiwa Ndejembi amejibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kiteto Mheshimiwa Edward Ole Lekaita aliyetaka kujua kwanini miji midogo ya Matui na Kibaya imekuwepo kwa muda mrefu bila kupandishwa hadhi amesema, uanzishwaji wa miji midogo hufanyika kwa kuzingatia Sheria ya Mipango Miji namba 8 ya mwaka 2007 pamoja na Mwongozo wa uanzishwaji wa maeneo ya utawala katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ya mwaka 2014 ambayo imeanzisha utaratibu na vigezo vinavyotakiwa kufuatwa.
Aidha, akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kibaha Viti Maalum Mheshimiwa Hawa Mchafu Chakoma na kuhusu Mji wa Kibaha kupandishwa hadi kuwa Manispaa Mheshimiwa Ndejembi amesema vigezo vya kuanzisha Manispaa ni pamoja na idadi ya watu katika Mji unaopendekezwa kuwa Manispaa ambapo kwa Mji wa kibaha na tayari Ofisi ya Rais TAMISEMI ilipokea ombi la kuipandishwa hadhi Mji huo kuwa Manispaa ambapo mpaka sasa maombi hayo yapo kwenye timu ambayo inapitia kuona kama inakidhi vigezo ili vya kupandishwa hadhi.