WAHAZINI NA WAHASIBU WATAKIWA KUSIMAMIA UKUSANYAJI WA MAPATO NA KUDHIBITI UPOTEVU WA FEDHA
Asila Twaha
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Angellah Kairuki amewataka Wahazini na Wahasibu wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kusimamia ukusanyaji wa mapato na kudhibiti upotevu wa fedha katika maeneo yao ya kazi ili kuiwezesha Serikali kupanga na kutekeleza malengo yake katika miradi ya maendeleo.
Mhe. Kairuki ametoa wito huo Agosti 17, 2023 kwa Wahazini na Wahasibu wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kikao kazi cha Ukaguzi wa Hesabu za Mwisho wa Mwaka wa Fedha 2022/23 kilichofanyika jijini Dodoma.
Akielezea umuhimu wa ukusanyaji wa mapato katika kupanga na kutekeleza miradi ya maendeleo kwenye sekta ya afya, elimu na miundombinu kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, Mhe. Kairuki amewahimiza maafisa hao kusimamia vyanzo vipya vya mapato vilivyoainishwa ikiwa ni pamoja na kuzuia mianya ya upotevu wa fedha.
“Wapo baadhi ya maafisa wanakengeuka kimaadili lakini kama Serikali tutendelea kuhimiza uadilifu ili watekeleze majukumu yao kwa kuzingatia Kanuni, Sheria, Taratibu na Miongozo iliyopo,” Mhe. Kairuki amesisitiza.
Ili kudhibiti upotevu wa mapato, Mhe. Kairuki ameagiza viongozi wenye dhamana ya kuteua mawakala kuzingatia vigezo na sifa stahiki ili kuwapata makawala watakaosimamia kikamilifu ukusanyaji wa mapato niaba ya Halamashauri.
Aidha, ameelekeza ukaguzi wa mashine za kukusanyia mapato ili kubaini ambazo hazifanyi kazi vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuchukua hatua stahiki.
Sanjari na hilo, amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi Idara ya Usimamizi, Ufuatiliaji na Ukaguzi (MMI) kuhakikisha wanasimamia hesabu zinafungwa vizuri ili kuepuka hoja za ukaguzi.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Wahazini Bw. George Masauri amesema kikao hicho kimewawezesha kubadilishana uzoefu wa kazi na kuwaongezea weledi hivyo ifikapo Agosti 31, 2023 Halmashauri zote 184 Tanzania Bara zitakua zimeshafunga hesabu.