WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na Sekta Binafsi katika utoaji elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi ili kuzalisha wataalamu wenye ujuzi wa kutosha unaohitajika katika sekta mbalimbali.
Pia, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa waajiri wote nchini waendelee kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha malengo ya kukuza ujuzi na kuongeza soko la ajira yanafanikiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa.
Ameyasema hayo jana (Ijumaa, Februari 24, 2023) katika hafla kati ya Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET) na wadau kutambua mchango wa uzalishaji wa rasilimaliwatu yenye ubora kwa soko la ajira. ”Maendeleo ya uchumi wa nchi yoyote yanategemea sana ngazi ya ujuzi wa nguvukazi uliyokuwa nayo. Hivyo, mchango wa wadau ni muhimu.”
Kadhalika, Waziri Mkuu amewapongeza waajiri kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa vitendo (field practical), uanagenzi, utarajali pamoja na namna wanavyoshiriki wenu katika kuandaa mitaala inayotumika kwenye vyuo na taasisi za Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
Amesema ushirikiano huo ni muhimu sana katika kuendeleza ujuzi kwa ajili ya kujenga uchumi wa viwanda. “Nataka nitumie fursa hii kuwapongeza lakini Serikali inatambua na inathamini juhudi mnazozifanya katika utoaji wa ajira kwa wahitimu wetu, tunawapongeza sana.”