WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo wahakikishe wanamfikisha katika vyombo vya sheria baba mzazi wa mwanafunzi wa darasa la pili (7) katika Kata ya Sokoni One mtaa wa Lonovono Jijini Arusha kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wake.
Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali inakemea vikali vitendo vya unyanyasaji, ubakaji na ulawiti kwa watoto, hivyo imewataka Wakuu wa mikoa na makamanda wa polisi nchini wahakikishe wanawasaka na kuwachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaobainika kujihusisha na vitendo hivyo viovu.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitofumbia macho na wala kukubaliana na vitendo vya ukatili kwa watoto, hivyo ameitaka jamii kushirikiana katika kupiga vita vitendo hivyo pamoja na kutowaficha wale wote wanaohusika na unyanyasaji huo.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Februari 17, 2023) baada ya kusambaa kwa taarifa kupitia vyombo vya habari vikimuonesha mtoto huyo ambaye anadaiwa kulawitiwa na baba yake mzazi. Mtoto huyo ambaye alisikika akielezea namna mzazi wake huyo alivyokuwa akimfanyia vitendo vya ukatili naye atafutwe na kupatiwa huduma ya matibabu kwa haraka.
Amesema katika siku za hivi karibuni kumeibuka tabia ya baadhi ya wazazi, walezi na wanajamii kuwafanyia watoto vitendo vya ukatili ikiwemo ulawiti, hivyo kuwasababishia maumivu makali pamoja na msongo wa mawazo hali inayowafanya baadhi yao kushindwa kuendelea na masomo. “Serikali haitosita kumchukulia hatua mzazi au mtu yeyote atakayebainika kufanya vitendo hivi vya ukatili.”
“Kumeibuka wimbi la ukatili wa kuwafanyia vitendo vya hovyo watoto wetu kwenye maeneo mbalimbali nchini, hivyo fanyeni uchunguzi na kubaini wanaohusika na vitendo hivyo. Wakuu wa Mikoa, Makamanda wa Polisi pamoja na Maafisa wa Ustawi wa Jamii hakikisheni mnawasaka watu wote wenye tabia hizo na kuwachukulia hatua.”
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa jamii ishirikiane na Serikali katika kutokomeza vitendo vya ukatili kwa watoto na wanawake