Habari

WAKUREGENZI WAPEWA SAA 48 KUPELEKA BENKI BILIONI 2.4 ILIYOKUSANYWA KUPITIA POS

0:00

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali Mhe. Deo Ndejembi (Mb) amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri ambazo zimekusanya mapato kupitia mfumo mpya wa TAUSI na hawajapeleka fedha benki kuhakikisha fedha hizo zinapelekwa ndani ya siku mbili ifikapo Juni 30,2023 kabla ya mwaka wa fedha 2022/23 kuisha.

Ndejembi ametoa maelekezo hayo leo tarehe 28, Juni 2023 katika Kikao na Idara ya Serikali za Mitaa kwa ajili ya kupokea taarifa ya hali ya ukusanyaji na usimamizi wa fedha katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.

Ndejembi amesema kufikia tarehe 25 Juni 2023 kiasi cha Shilingi bilioni 2.4  zilizokusanywa kupitia POS katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato wa TAUSI kwenye halmashauri zilikuwa hazijapelekwa benki lakini kwenye mfumo zinaonekana zimekusanywa.

“Wakati napitia taarifa nimeona bilioni 2.4 ambayo inaonekana kwenye mfumo imekusanywa lakini haijapelekwa benki, sasa niwatake Wakurugenzi wote ambao wamekusanya lakini haijapelekwa benki , kupeleka fedha hizo ndani ya siku mbili hizi kabla ya mwaka wa fedha kuisha”

Aidha, Ndejembi ameziagiza Halmashauri 103 ambazo hazijafanya usuluhishi wa Kibenki (Bank Reconciliation) ambao unatakiwa kufanyika ndani ya siku 15 baada ya mwezi kwisha kuhakikisha wanafanya usuluhishi wa Kibenki  ndani ya siku mbili ili kuepuka hoja za CAG.

Ndejembi amesema Mkurugenzi yeyote atakayeshindwa kutekeleza maagizo hayo ndani ya Siku mbili kabla ya mwaka wa fedha kwisha atoe maelezo kwa maandishi Kwanini hajatekeleza na kwanini asichukuliwe hatua kali.

Kadhalika, Ndejembi amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha fedha zote zinazikusanywa katika Halmashauri kuanzia ngazi ya vijiji, mitaa, kata na huduma za Afya na Elimu kuingizwa kwenye mfumo ili kuongeza ufuatiliaji wa fedha hiyo.

Back to top button