Habari

SMZ KUMALIZA ZAMU ZA WANAFUNZI ZANZIBAR

0:00

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inakaribia kumaliza ujenzi wa madarasa 5,000  kuondoa zamu mbili  kwa wanafunzi nchi nzima na kubakisha zamu moja.

Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipofungua rasmi Skuli mpya ya Sekondari Tumekuja iliopo Mwembeladu Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi tarehe: 09 Januari 2024 katika shamrashamra za Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Vilevile Skuli  hiyo mpya ya Tumekuja ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,755 kwa wastani wa uwiano wa wanafunzi 45 kwa darasa moja, tayari wanafunzi wameshapangwa wiki ijayo kuanza masomo.

Rais Dkt.Mwinyi amempongeza mkandarasi wa kampuni ya CRJE kwa kujenga Skuli ya kisasa ambayo ina maabara tatu ya kisasa, chumba cha kompyuta, maktaba na ukumbi wa mikutano.

Aidha Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa  Serikali itaendelea kujenga maghorofa katika sekta ya elimu kwa wanafunzi kutozidi 45  kwa darasa moja .

Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali itaendelea kufanya uamuzi sahihi kwa faida ya nchi na kuyakarabati majengo ya mji mkongwe kwani ni urithi wa nchi  kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

Kwa upande mwingine Rais Dkt.Mwinyi amesema mafanikio yaliyopatikana katika elimu ni kwa juhudi za  Waalimu kwa kuongeza idadi ya ufaulu ikiwemo kutoka wanafunzi 2,000 hadi 6,000 Skuli za Msingi na matokeo ya kidato cha sita ya mwisho ufaulu wa daraja la kwanza hadi daraja la tatu kwa asilimia 90.

Back to top button