SMZ KUJENGA HOSPITALI MPYA KILA MKOA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha huduma za afya ngazi zote na imekamilisha ujenzi wa hospitali za Wilaya na itajenga hospitali mpya kwa kila mkoa Zanzibar.
Rais Dkt.Mwinyi amesema hayo alipofungua jengo jipya la huduma za matibabu ya dharura na maabara ya kisasa katika kituo cha afya Makunduchi, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja tarehe: 17 Januari 2024.
Aidha Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa mwaka wa fedha 2023/24 Serikali imeendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya ngazi ya msingi kwa kujenga majengo mapya, kuweka vifaa vya kisasa kwa lengo la kutoa huduma za uchunguzi na dharura.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amesema Serikali imelenga kuzisogeza huduma zote muhimu za afya kuwa karibu na wananchi ikiwa pamoja na kuweka mifumo ya tehama, upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ili kurahisisha huduma za matibabu na uchunguzi kwa wakati wote .