Habari

RAIS SAMIA HATAKI MISUKOSUKO KWA WAFANYABIASHARA

0:00

 

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua kama mlezi wa Sekta binafsi nchini na hataki kuona wafanyabiashara  wanapata misukosuko wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Amesema maono ya Rais ni kujenga sekta binafsi itakayokuwa na mchango mkubwa zaidi kwenye pato la Taifa na ili kufikia azma hiyo, viongozi wengine wahakikishe nia njema ya Rais kwa Wafanyabiashara inatekelezwa kwa vitendo.

Aidha, Dkt. Biteko amewaagiza watendaji wa Serikali kuhakikisha  wanailea Sekta binafsi na kila mtu atimize wajibu wake kwenye eneo lake “kama wewe ni Afisa wa TANESCO uliye na wajibu wa kumuunganishia mfanyabiashara umeme ambao mwisho wa siku ataulipia kwa ajili ya mapato yako, huna sababu ya kumwambia njoo kesho wakati kazi hiyo ungeifanya leo.”

Amesema Watendaji ambao ni warasimu lazima waone aibu kwa kuchelewesha shughuli zinazoijenga nchi.

Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia anataka kuona watanzania wakiwa kwenye daraja la kwanza katika nchi yao na pia waweze kufanya uwekezaji ndani na nje ya nchi bila vikwazo vyovyote.

Kuhusu Sekta ya Utalii nchini, amesema bado kuna changamoto ya upungufu wa vitanda kwa wageni wa ndani na nje ya nchi hivyo bado kuna kazi kubwa ya kuwekeza kwenye sekta ya ‘hospitality’ ambapo amewapongeza wamiliki wa Rafiki hoteli na wawekezaji wengine ambao wanaifanyia kazi changamoto hiyo.

Back to top button