“NIMERIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA MRADI WA EBARR KISHAPU” DR. MKAMA
Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Dr. Switbert Mkama amesema ameridhishwa na usimamizi na utekelezaji wa Mradi ya Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi kwa Kutumia Mfumo Mfumo Ikolojia Vijijini (EBARR) katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga.
Amesema hayo alipofanya ziara ya kukagua mradi wa mashine za kukoboa na kusaga nafaka, madume bora ya ng‘ombe aina ya borani na hatua za uchimbaji wa malambo zilizopo katika vijiji vya Kiloleli na Muguda wilayani humo tarehe 12 Agosti 2023.
Akizungumza kwa nyakati tofauti wakati wa ziara hiyo, Dkt. Mkama ametoa wito kwa wananchi wilayani humo kuitunza miradi hiyo ambayo inakelezwa kwa lengo la kusaidia katika utunzaji wa mazingira na kukabiliana na ukame kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Ndugu zangu naomba niwaambie miradi hii inayoletwa hapa kwenu na maeneo mbalimbali itawasaidia katika kujipatia kipato kwa kufanya shughuli mbalimbali zikiwemo ufugaji nyuki, zitawasaidia kuacha shughuli zinazoharibu mazingira zikiwemo ukataji miti na kuchoma mkaa na mkipata fedha mtanunua majiko banifu na ya gesi,“ amesema.
Aidha, Dkt. Mkama amewahimiza viongozi na wananchi wilayani humo kuhakikisha shughuli zote za mradi zinakamilika Desemba 2023 wakati mradi utakapofikia ukingoni pamoja na kuufanya kuwa endelevu iweze kuwanufaisha kwa vizazi vijavyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kishapu Mhe. Boniphace Butondo ameishukuru Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kutekeleza Mradi wa EBARR akisema kwamba mradi huu umekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wilayani humo.
Amesema miradi mbalimbali ikiwemo malambo, mifugo, kiwanda kidogo cha uchakataji wa ngozi ambacho kinahusisha kikundi cha ushonaji wa viatu na unenepeshaji wa mifugo unakwenda kuinua ufugaji wilayani humo.
Pia, mbunge huyo amesema kuwa mashine za kukamua alizeti zinazotarajiwa kutolewa kupitia mradi huo zitaweza kuwasaidia wakulima wa zao hili kupata fursa ya kukamua mafuta na hivyo kuinua uchumi wa wilaya.
Shughuli hizo zinazotekelezwa kupitia Mradi wa EBARR wilayani Kishapu zinagharimu shilingi bilioni 1.6 ambapo mradi huo unatekelezwa katika Kata ya Kiloleli inayohusisha vijiji vya Kilollei na Muguda na Kata ya Lagana katika vijiji vya Mihama na Beledi.
Mradi huo unaofadhiliwa na Mfuko wa Nchi zinazoendelea kupitia Mfuko wa Dunia wa Mazingira (GEF) unatekeleza pia katika wilaya za Simanjiro (Manyara), Mvomero (Morogoro), Mpwapwa (Dodoma) na Kaskazini ‘A’ Unguja (Zanzibar),