DKT. MSONDE AKAGUA UJENZI WA MADARASA SHULE YA MSINGI SANINIU LAIZER
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais TAMISEMI (Elimu), Dkt. Charles Msonde ametembelea na kukagua ujenzi wa miundombinu katika Shule ya Msingi Saniniu Laizer iliyojengwa na mchimbaji mdogo wa Madini ya Tanzanite, Saniniu Laizer katika Kijiji Cha Naepo, wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara.
Msonde ametembelea shule yenye mchepuo wa kingereza kwa ajili ya kujionea hali ya utoaji elimu ikiwa ni pamoja na kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa ya Awali na vyoo vinavyojengwa na Serikali kupitia Mradi wa BOOST.
“Ndugu yangu Saniniu Laizer tunakushukuru kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha utoaji wa elimu nchini kwa kujenga shule na nyumba za watumishi, ambayo inasaidia wanafunzi kupata elimu katika maeno haya” amesema Dkt. Msonde
Aidha, Dkt. Msonde amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo, na ndio maana inaendelea kuboresha shule hiyo kwa kutoa shilingi milioni 64 kujenga vyumba viwili vya madarasa ya kisasa ya darasa la Awali na matundu sita ya vyoo.
Amesema Serikali itaendelea kujenga miundombinu na kuleta Watumishi katika shule hiyo kulingana na uhitaji ili shule iendelee kutoa elimu bora kulingana na maono ya Saniniu Laizer ya shule hiyo kufundisha lugha ya kingereza.
Kadhalika, Dkt. Msonde amewashukuru Wananchi wa Kata ya Naisinyai kwa kushiriki katika ujenzi wa nyumba vya madarasa ambapo walijitoa kuchimba Msingi, kuleata Mawe na Vifusi katika eneo la ujenzi.
Ikumbukwe kuwa, Shule ya Msingi Saniniu Laizer inamilikiwa na Serikali na ina Jumla ya wanafunzi 159.