Habari

MAJALIWA ATAKA UWEKEZAJI ATCL UWE KICHOCHEO CHA UKUAJI WA UCHUMI

0:00

 

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa ameitaka Wizara ya Uchukuzi kusimamia ipasavyo Shirika la Ndege Tanzania ili kuhakikisha uwekezaji mkubwa uliofanywa unaleta matokeo chanya na kuwa kichocheo cha ukuaji wa sekta nyingine mtambuka na uchumi kwa ujumla wake.

Amesema kuwa ongezeko la ndege na huduma za usafiri inasaidia kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania na mataifa mengine kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuongeza idadi ya watalii wanaokuja nchini.

Amesema hayo leo (Jumanne, Machi 26, 2024) alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mapokezi ya ndege mpya aina ya Boeing 737-9 Max, kwenye uwanja wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam.

Aidha Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa ili kuendelea kuikuza sekta ya anga nchini, Wizara ya Uchukuzi iandae mpango wa kuongeza wataalamu wazalendo katika fani zinazohusu masuala ya ndege hususan katika eneo la matengenezo na urubani.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa Shirika la Ndege Tanzania kuongeza uzalendo na kuwafichua wale wote wenye nia ya kulihujumu shirika hilo pamoja na kudhibiti upotevu wa mapato kupitia tiketi na mizigo.

Pia, Amewataka viongozi na watendaji wa Shirika hilo wahakikishe ndege zote zinaendeshwa kwa tija kwa kufanya tafiti  za kutosha wa masoko kabla ya kupeleka ndege

Amesema kuwa usafiri wa anga umekuwa chachu ya kuongeza mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo na biashara. “Uwepo wa usafiri wa ndege umeongeza tija kubwa kwa wakulima hususan wa mazao ya mbogamboga na matunda, wafugaji na wafanyabiashara wa Kitanzania”

Katika Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya sita imesaini mikataba ya miradi mipya 6 yenye thamani ya Shilingi Bilioni 674.3 inayohusu ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli (shipyard) katika Ziwa Tanganyika, ujenzi wa meli kubwa ya kubeba mizigo tani 3,500 na meli nyingine yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 za mizigo ambayo inajengwa katika Ziwa Victoria.

Back to top button