MAJALIWA AKAGUA MRADI WA MAJI KOMUGE
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia amedhamiria kuendelea kutekeleza kampeni yake ya kumtua ndoo mama kichwani ili kuwezesha kila mtanzania kupata huduma ya maji safi na salama karibu na maeneo yao.
Amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita ipo imara na itaendelea kuwahudumia kwenye mambo yote ya msingi ambayo ni mahitaji ya kila siku ikiwemo afya, maji, barabara na elimu.
Amesema hayo leo (Jumatano Februari 28, 2024) wakati alipokagua mradi wa maji wa Komuge uliopo Halmashauri ya wilaya ya Rorya mkoani Mara.
Aidha Mheshimiwa Majaliwa amewataka watumishi wa Halmashauri zote nchini kuwa na utaratibu wa kufanya ziara kwenye maeneo yao ili wasikilize changamoto za wananchi na kuzifanyia kazi.
Kwa upande wake Waziri wa Maji Jumaa Aweso amesema kuwa ndani ya wiki hii Shilingi milioni 720 zitatolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji Komuge ili ndani ya miezi mitatu uwe umekamilika” mhandisi wa maji mkoa na wilaya anzeni kusafisha eneo kwa ajili ya eneo ambalo litajengwa tenki”.