Habari Tofauti

HALMASHAURI 5  KUWAJIBIKA KWA KUTOTENGA FEDHA ZA AFUA ZA LISHE

Angela Msimbira 

0:00

WAKURUGENZI wa Halmashauri tano ambao hawakutimiza mpango wa utengaji fedha za kutekeleza afua za lishe kulingana na idadi ya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano watakiwa kuhakikisha wanatenga fedha hizo kabla ya Desemba mwaka huu.

Maagizo hayo yametolewa leo Agosti 29,2023 jijini Dodoma na Waziri wa  Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki wakati wa kufungua mkutano wa mwaka wa tathimini ya saba ya Utekelezaji wa mkataba wa lishe Nchini.

Amesema Wakurugenzi wa Halmashauri tano za Mpanda DC, Kasulu DC, Mkalama DC, Uyui DC na Lushoto DC ambazo katika mipango yao hawakuzingatia kiasi cha fedha kulingana na idadi ya Watoto chini ya miaka mitano watekeleze haraka maelekezo yaliyotolewa ifikapo Desemba, 2023 wakati wa kufanya mapitio ya bajeti.

“Kuanzia sasa naelekeza Halmashauri yoyote ambayo itakuwa haijatoa pesa zote, bakaa itakuwa deni la Halmashauri husika na itabidi iongezwe kwenye bajeti ya mwaka unaofuata, hii ni kuhakikisha ifikapo 2025, Mamlaka za Serikali za Mitaa tuwe tumefikia kiasi cha shilingi bilioni 67 ambazo tunatakiwa kuchangia kutekeleza Mpango Jumuishi wa Pili wa Lishe wa Taifa ambayo ni asilimia 10 ya bajeti yote ya lishe nchini kwa kipindi cha miaka mitano.” Amesema Mhe Kairuki

Mhe.Kairuki ametoa rai kwa wakuu wa Mikoa kusimamia Halmashauri zao kwa kuhakikisha fedha iliyopangwa kutekeleza afua za lishe zinatolewa kwa wakati.

“Hii inatokana na matokeo niliyo nayo ambayo inaonekana kuwa kiashiria hiki bado hakitekelezwi ipasavyo katika maeneo mengi.

Wakurugenzi wa Halmashauri wahakikishe kuwa fedha zinazotolewa zinaenda kutekeleza shughuli zilizopangwa na sio vinginevyo.” amesisitiza Mhe Kairuki

Amesema Ofisi ya Rais -TAMISEMI itaendelea kuimarisha usimamizi na ufuatiliaji ili kuwabaini wanaofanya udanganyifu katika matumizi ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya utekelezaji wa afua za lishe

Back to top button