RAIS DK.MWINYI ASEMA ZANZIBAR IKO TAYARI KUPOKEA MABADILIKO YA TEKNOLOJIA
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi amesema Serikali imejiandaa kuhakikisha Zanzibar inakuwa mstari wa mbele kuyapokea mabadiliko ya teknolojia ambayo ni msingi muhimu kwa kukuza na kuendeleza uchumi wa kisasa pamoja na kurahisisha maisha ya wananchi wa hali zote.
Ameyasema hayo leo katika hafla ya uzinduzi wa Mkakati wa kidijitali wa Serikali na Mfumo wa Bajeti na Matumizi Serikalini (BAMAS) uliyofanyika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Aidha Rais Dk.Mwinyi amesema matumizi ya mifumo ya TEHAMA yataleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii katika utendaji kazi wa Serikali kwa ulazima wa kutumia mifumo hiyo kwa kuwa matumizi ya TEHAMA yataimarisha ukusanyaji wa mapato, kurahishisha utoaji wa huduma sekta ya Afya, Elimu , kudhibiti matumizi ya fedha za umma, kukomesha vitendo vya wizi, kuzuia rushwa na ubadhirifu pamoja na kuimairisha usalama wa nchi.
Vile vile amesema mfumo wa BAMAS umeleta uwazi kwenye matumizi Serikalini, utaimarisha uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali, umewezesha mifumo yote ya malipo na matumizi ya fedha za Serikali kusomana kwa haraka na kwa ufanisi na kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili kuwaletea wananchi maendeleo.