WAZIRI MKUU amesema Serikali ya Urusi imeahidi kushirikiana na Afrika kuboresha uchumi ikiwemo Tanzania.
“Mwelekeo wa mkutano wa jana ilikuwa ni kuona namna gani tunaweza kuboresha uchumi wa nchi za Afrika kwa pamoja na Urusi. Wao wametoa mwelekeo wa namna ambavyo wataweza kushirikiana na nchi za Afrika kuboresha uchumi wa kila nchi na sisi tumeeleza mkakati wa kiuchumi kwenye nchi yetu ambao Rais Putin ameuridhia.
Aliyasema hayo (Ijumaa, Julai 28, 2023) baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi ambako alimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mkutano huo umefanyika kwenye kituo cha mikutano na maonesho cha Expo Forum, jijini St. Petersburg, Urusi. Akizungumza.
Waziri Mkuu amesema Tanzania itaendelea kuimarisha miundombinu ya usafirishaji kwa lengo la kuboresha uchumi na biashara kwa kutumia rasilmali zake ikiwemo madini, maliasili na kilimo hasa upatikanaji wa mbolea. “Tumesisitiza pia matumizi ya nishati mbadala kama njia muhimu ya kuwawezesha wananchi wa vijijini ili nao wamudu kutumia nishati mbadala kukuza uchumi wao,” amesema.
Amelitaja eneo jingine kuwa ni kukuza biashara ya mazao baina ya Afrika na Urusi ambapo yenyewe inaweza kuwa soko la moja kwa moja ama kwa kuwatumia marafiki zake. “Ili kufikia hayo, jitihada za kila nchi kwenye kilimo zimesisitizwa. Tanzania tumeeleza mkakati wa kukuza kilimo ikiwemo umwagiliaji. Pia tunahitaji mbolea, madawa na vitendea kazi ili tufanikiwe kwa kasi zaidi.”
Waziri Mkuu aliwaeleza viongozi hao wa Afrika juu ya Mkakati wa Rais Dkt Samia wa kutoa elimu bure na vifaa vya kufundishia kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wazazi.
Mapema, akifungua mkutano huo, Rais wa Urusi, Vladmiri Putin alisema nchi za Afrika zimekuwa na mahusiano mazuri na ya muda mrefu na Urusi na kwamba nchi hiyo imekuwa ikiendelea kutoa misaada bila vikwazo kwenye maeneo mbalimbali.