WASIMAMIZI WA ELIMU WATAKIWA KULETA MATOKEO CHANYA
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Adolf Ndunguru amewataka wasimamizi wa elimu katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha utendaji kazi ili kuleta matokeo chanya yaliyokusudiwa na serikali kwa ngazi zote za elimu.
Ndunguru ameyasema hayo Juni 28, 2023 wakati akifunga mafunzo ya matumizi ya njia na vifaa vya mtaala wa elimu ya awali vilivyoboreshwa kwa walimu wa elimu ya awali yaliyofanyika katika Chuo cha ualimu mkoani Morogoro.
Amewaelekeza Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha mafunzo ya walimu wanaofundisha elimu ya awali yanaendeshwa kwa ukamilifu na ufanisi kwenye vituo vyote 22 vilivyochaguliwa kama ilivyopangwa.
“Walimu wote wanaopatiwa mafunzo wanaporudi vituoni waendelee kupangiwa kufundisha madarasa ya elimu ya awali ili ujuzi wao uendelee kutumika na lengo la kuboresha ujifunzaji wa mwanafunzi wa elimu ya awali lifikiwe,”amesema.
Amesema kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) mwaka 2022/23 Serikali imetoa Sh.bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za msingi 302 zenye vyumba vya madarasa vya mfano vya elimu ya awali, vyumba vya madarasa 2,929, madarasa ya awali ya mfano 368 yanajengwa kwenye shule zilizopo ili kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani.
Naye, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Elimumsingi na Awali kutoka TAMISEMI, Susana Nussu amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa mradi wa BOOST na yatahusisha washiriki 4,240 wakiwemo wawezeshaji wa kitaifa 110, walimu wanaofundisha elimu ya awali 3000, Walimu wakuu 552 na Maafisa Elimu kata 552.